Mali ambayo thamani yake haijulikani imeteketea katika soko la Mutindwa huko Makadara.
Wafanyabiashara wanasema moto huo ulioanza kwenye kibanda kimoja saa nane usiku wa kuamkia leo Jumatano ulienea kwa kasi hadi vibanda vilivyopo karibu na kuteketeza soko lote.
Timu ya zimamoto kutoka kaunti ya Nairobi iliwasili sokoni hapo lakini haikuweza kuokoa chochote.
Wafanyabiashara wanasema moto huo ungedhibitiwa ikiwa jitihada zaidi zingefanywa.
Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenye aliyezuru soko hilo alitaka uchunguzi wa haraka kufanywa kuhusiana na kuzuka kwa moto huo na kulitaka bunge la kaunti ya Nairobi kujadili visa vya mioto vya hivi karibuni ambavyo vimekuwa vikitokea katika masoko mbalimbali katika kaunti hiyo.
Mwenje aliongeza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kusaidiwa katika jitihada za ujenzi mpya na kutoa wito wa utulivu wakati polisi wakichunguza chanzo cha moto huo.