Waziri mteule wa Fedha John Mbadi, amesema ataelekeza juhudi zake katika kufanyia mabadiliko Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru nchini KRA, kuhakikisha inakusanya mapato yatakayowezesha serikali kuendesha mipango yake.
Kulingana na Mbadi aliyefika mbele ya kamati ya bunge kuhusu uteuzi Jumamosi asubuhi, suluhu kuhusu nakisi ya mapato sio kuongeza ushuru, lakini ni kuimarisha ukusanyaji ushuru.
“Mengi yamesemwa kuhusu ukusanyaji ushuru, huku lengo kuu likiwa kuongeza ushuru, na kubuni aina mpya za ushuru. Sidhani hilo ni suluhu. Suluhu kuhusu ukusanyaji ushuru ni kuimarisha halamashauri ya KRA,” alisema Mbadi.
Iwapo uteuzi wake utaidhinishwa, waziri huyo mteule alisema atawekeza pakubwa kwa mifumo ya KRA, kuhakikisha inaafikia na kupitisha kiwango cha mapato. Alisema hatua hiyo itafanikishwa na kupiga msasa uwezo wa wafanyakazi wa KRA kuhusu uwezo wao wa kutekeleza majukumu.
“Halmashauri ya KRA nisawa na ng’ombe tunayemkamua lakini halishwi. Asilimia 2 ya mapato yetu yanafaa kutumiwa kuimarisha umwezo wa KRA, lakini hatufanyi hivyo,” alidokeza Mbadi.
Kulingana na Mbadi, taifa hili hupoteza mapato mengi kutokana na mifumo hafifu ya kukabiliana na wanaokwepa kulipa ushuru.
Mbadi ni mmoja wa viongozi watano kutoka upinzani ambao wameteuliwa na Rais William Ruto katika Baraza Jumuishi la Mawaziri, baada ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.