Gor Mahia maarufu Sirkal wametanua uongozi wa alama nane kileleni pa jedwali la ligi ya FKF, baada ya kusajili ushindi wa bao moja kwa nunge ugenini dhidi ya Nairobi City Stars katika mechi ya raundi ya 22 iliyopigwa Jumamosi uwanjani Kenyatta kaunti ya Machakos.
Benson Omalla alitikisa nyavu kunako dakika ya nne akiunganisha pasi ya Shaiff Musa na kusajili ushindi wa kwanza tangu walipoibwaga Tusker FC Januari 20 mwaka huu.
Katika matokeo mengine Posta Rangers wamedumisha nafasi ya pili baada ya kuwalaza Ulinzi Stars bao moja bila jibu katika uwanja wa Police Sacco,Muranga Seal wakaikaanga Bidco united kwa goli moja kwa sifuri, wakati Bandari FC wakikosa adabu za mgeni wakiwaadhibu Nzoia 2-1 kiwarani Sudi.
Masaibu y Shabana FC yameongozeka baada ya kuzamishwa bao moja kwa bila dhidi ya wenyeji Police FC.
Gor wanaongoza jedwali kwa alama 47 ,wakifuatwa na Rangers,Bandari na City Stars kwa alama 37 kila moja.