Home Taifa Siku ya kuzungumza Kiswahili nchini kutengwa

Siku ya kuzungumza Kiswahili nchini kutengwa

0
kra

Waziri wa masuala ya jinsia, utamaduni, sanaa na turathi nchini Aisha Jumwa amesema kwamba serikali huenda ikatenga siku ya kuzungumza lugha ya Kiswahili.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la pili la kimataifa la kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki, waziri Aisha alisema kwamba lengo kuu la kutenga siku hiyo ni kukuza lugha hiyo.

kra

Alifichua kwamba mchakato wa kubuni tume ya kitaifa ya Kiswahili umefikia hatua za mwisho mwisho na itajukumiwa kuunda sera za kimkakati za kuhakikisha Kiswahili kinakuzwa na kuendelezwa nchini.

Jumwa alisema siku hiyo itakapotengwa, wakenya wote akiwemo Rais, Majaji, wafanyakazi wa serikali, wanafunzi na walimu shuleni watahitajika kutumia Kiswahili pekee katika kazi zao siku hiyo.

Katika kikao hicho kilichofanyika huko Mombasa kabla ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili ulimwenguni yaliyoandaliwa jana, Jumwa alisema kwamba kwa sasa zaidi ya watu milioni 200 wanazungumza lugha hiyo ulimwenguni.

Kulingana naye hiyo ni ishara kwamba juhudi za kukuza na kueneza lugha hiyo zinazaa matunda.

Siku ya Kiswahili ulimwenguni huadhimishwa Julai 7 kila mwaka na ilianzishwa na shirika la umoja wa mataifa la sayansi na utamaduni UNESCO mwaka 2022.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutangaza mwaka 1954 alipokuwa kiongozi wa chama cha TANU kwamba lugha ya Kiswahili itakuwa lugha itakayounganisha waafrika katika kutafuta uhuru.

Website | + posts