Home Habari Kuu Sierra Leon yapiga marufuku ndoa za mapema

Sierra Leon yapiga marufuku ndoa za mapema

0
kra

Sierra Leone imeanzisha sheria mpya ya kupiga marufuku ndoa za utotoni kwa mbwembwe nyingi katika sherehe iliyoandaliwa na mke wa Rais Fatima Bio katika mji mkuu, Freetown.

Wageni waalikwa, wakiwemo wake wa marais kutoka Cape Verde na Namibia, walitazama jinsi mumewe Rais Julius Maada Bio akitia saini mswada wa Marufuku ya Ndoa za Utotoni kuwa sheria.

kra

Mtu yeyote ambaye sasa atahusika katika ndoa ya msichana aliye na umri wa chini ya miaka 18 atafungwa jela kwa takriban miaka 15 au kutozwa faini ya karibu $4,000 (£3,200), au zote mbili.

Mwanafunzi wa chuo kikuu Khadijatu Barrie, ambaye dadake aliolewa akiwa na umri wa miaka 14, aliambia BBC kuwa alifurahishwa na marufuku hiyo lakini akatamani ilianza mapema ili kumwokoa mdogo wake.

“Natamani sana ingeanza mapema. Angalau ningeweza kumuokoa dada yangu na marafiki zangu na majirani wengine,” mhitimu huyo wa masomo ya jinsia mwenye umri wa miaka 26 alisema.

Sierra Leone ni jamii ya mfumo dume na ni kawaida kwa baba kumtoa bintiye kwa ndoa ya lazima.

Bi Barrie alikabiliana na hali hiyo akiwa na umri wa miaka 10. Alikataa na kutoroka nyumbani baada ya babake kumkataa.

Alipata bahati ya kupata walimu waliomlipia karo ya shule na mfanyakazi mwenye huruma kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ambaye alimsaidia kwa kumpa mahali pa kuishi.

Lakini anasema ni vigumu kwa wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini kupinga mila hiyo na kila jamii itahitaji kufahamishwa kuhusu sheria hiyo mpya ili kuanza kutekelezwa kwa ufanisi.

“Ikiwa kila mtu ataelewa kile kinachokungoja utakapofanya hivyo, nina uhakika nchi hii itakuwa bora,” Bi Barrie alisema.

Wizaŕa ya afya inakadiria kuwa thuluthi moja ya wasichana wanaolewa kabla ya kufikisha miaka 18, na hivyo kusababisha idadi kubwa ya vifo vya uzazi nchini humo – miongoni mwa vifo vya juu zaidi duniani.

Wale wanaokabiliwa na adhabu chini ya sheria hizo mpya ni pamoja na bwana harusi, wazazi au walezi wa mtoto harusi, na hata wale wanaohudhuria harusi.