Home Habari Kuu Ruto: Waliopanga maandamano wanapaswa kuwaomba Wakenya msamaha

Ruto: Waliopanga maandamano wanapaswa kuwaomba Wakenya msamaha

0

Rais William Ruto amewataka waliopanga maandamano ya hivi karibuni kuwaomba Wakenya msamaha.

Amesema ni ukosefu wa uaminifu kwa upinzani kusingizia kujali maslahi ya watu ilhali walichochea maandamano yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali.

“Wanapaswa kuaibika,” alisema Rais Ruto.

Aliyazungumza hayo leo Ijumaa wakati wa kuzinduliwa kwa Soko la Samaki la Kichwa Cha Kati mjini Malindi.

Kadhalika alitoa hundi kwa jamii ya uvuvi ya eneo hilo katika kaunti ya Kilifi.

Mawaziri Aisha Jumwa, Salim Mvurya, Kindiki Kithure, Soipan Tuya, Spika wa Seneti Amason Kingi na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro ni miongoni mwa waliokuwapo.

Rais Ruto aliwahakikishia Wakenya kuwa siasa za Kenya hazitakumbwa tena na vurugu.

Alisema serikali itaweka hatua kali za kulinda maisha na mali ya Wakenya.

Kiongozi wa nchi alisema itakuwa ni usaliti kwa watu ikiwa wanasiasa watatoa kipaumbele kwa maslahi yao.

“Wakati wa siasa umepita, ni wakati wa kuwahudumia Wakenya,” aliongeza Rais Ruto.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Salim Mvurya alisema Rais hatashiriki mazungumzo yasiyokuwa ya kikatiba na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

“Tunataka mazungumzo yafanywe ndani ya misingi ya katiba,” alisema Waziri Mvurya.

Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichungw’ah alisema mazungumzo, ikiwa kuna yoyote yatakayofanyika kati ya Rais Ruto na Raila, yanapaswa kuangazia masuala yanayowakumba Wakenya.

Kulingana naye, hakuna haja ya mpatanishi wa kigeni kusimamia mazungumzo juu ya masuala yanayowaathiri Wakenya.

“Ikiwa mtakayozungumza yanawahusu raia, basi mazungumzo yanapaswa kufanyika hadharani katika kikao cha umma,” alisema Ichungw’ah.

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alitoa wito kwa wakazi kujiepusha na maandamano ya vurugu yanayotishia uthabiti wa kiuchumi wa kaunti hiyo.

“Kilifi ni kaunti ya watalii, mkijihusisha katika maandamano ya vurugu, watalii wataondoka,” alionya Mung’aro.

Baadaye mjini Kilifi, Rais alizindua jengo la usimamizi wa shule, madarasa mawili na maabara mbili katika shule ya upili ya wasichana ya St. Thomas.

Alisema elimu ya wasichana ina nguvu ya kubadilisha jamii na kuangamiza ukosefu wa usawa wa jinsia.

Rais Ruto yuko kwenye ziara ya siku tano katika eneo la Pwani iliyoanza jana Alhamisi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here