Serikali ya kaunti ya Nairobi , imetangaza mipango ya kujenga madarasa 114 mapya, kwenye taasisi za Chekechea (ECDE), katika wadi zote 85, ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Hatua hiyo inafuatia azimio la mkutano wa baraza la 34 la mawaziri wa kaunti hiyo, ulioandaliwa jumanne, kwa lengo la kupanua miundombinu hususan katika shule za umma..
Kulingana na taarifa kutoka serikali ya kaunti ya Nairobi, madarasa hayo yatasaidia pakubwa kupunguza msongamano wa wanafunzi unaoshuhudiwa katika shule za umma, kufuatia kuanzishwa kwa mpango wa kuwapa wanafunzi lishe shuleni almaarufu ‘Dishi Na County’.
“Vituo vya elimu ya chekechea vimepokea wanafunzi kupita kiasi. Ujenzi wa madarasa hayo hatutapunguza tu msongamano, lakini pia utahakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu bila malipo,” ilisema taarifa ya kaunti hiyo.
Madarasa hayo mapya pia yanalenga kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za chekechea.