Home Kaunti Shule ya wasichana ya Tipet yawapa tumaini wanaokwepa ukeketaji na ndoa za...

Shule ya wasichana ya Tipet yawapa tumaini wanaokwepa ukeketaji na ndoa za mapema

Shule ya upili ya wasichana ya AGC Tipet iliyoko kaunti ya Pokot Magharibi imekuwa ishara ya matumaini kwa wasichana wengi wanaokwepa ukeketaji na ndoa za mapema.

Wasichana wengi ambao waliacha shule kwa sababu ya ukosefu wa karo pia wamepata nafasi katika shule hiyo.

Hata ingawa inakumbwa na changamoto kadhaa zikiwemo za miundomsingi, shule hiyo inaendelea kukua kila kuchao.

Ili kuifikia ni lazima uvuke mto Turkwel hatua ambayo ni changamoto kwa wadau wote wakiwemo wanafunzi na walimu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Effie Mugalo, ‘alisisitiza kuhusu kujitolea kwao kuhudumu kama eneo la uokozi wa mtoto msichana.

Wengi wa watoto hao wamekubaliwa kuishi shuleni humo na kupata elimu hata bila kulipa karo na bila sare.

Effie anasema shule hiyo imekuwa kimbilio kwa wasichana wengi tangu kuasisiwa na idadi ya wanafunzi imeongezeka mara dufu na sasa wanafunzi ni 150.

Changamoto kuu kulingana naye ni ufadhili na usimamizi vitu ambavyo anasema vinalemaza uwezo wa shule hiyo kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Wasichana wengi katika shule hiyo hawana stakabadhi muhimu kama vyeti vya kuzaliwa hali inayofanya iwe vigumu kuwasajili kwenye tovuti ya NEMIS ili wahesabiwe kati ya wanaofadhiliwa na serikali kuu.

Shule hiyo ina walimu watatu tu walioajiriwa na tume ya TSC huku wengine wakiwa wa kujitolea ili kujazilia kwani shule haina uwezo wa kifedha wa kuajiri walimu waliohitimu.

Madarasa ambayo ujenzi wake bado haujakamilika ndiyo yanatumika shuleni humo huku yakigeuzwa kuwa mabweni usiku.

Kando na mabweni, shule hiyo inahitaji maabara na maktaba ili wanafunzi waweze kupata mazingira mazuri ya kuafikia ndoto zao.