Home Kaunti Shule ya Makere huko Tana River katika hatari ya kuathiriwa na mto...

Shule ya Makere huko Tana River katika hatari ya kuathiriwa na mto Tana

0

Huku shule zikifunguliwa leo kwa muhula wa pili, shule ya msingi ya Makere katika eneo bunge la Galole kaunti ya Tana River, iko katika hatari ya kuzamishwa na maji ya mto Tana.

Shule hiyo iliyo na wanafunzi wapatao 1200 iko umbali wa mita 20 tu kutoka kwa mto huo. Tangi la maji, jiko la shule, nusu ya uzio wa shule, uwanja wa soka pamoja na afisi ya chifu wa eneo hilo ni baadhi ya maeneo yaliyojaa maji ya mto Tana.

Darasa la chekechea linasemekana kuwa umbali wa mita 14 kutoka kwa mto Tana huku maji yake yakiendelea kusambaa katika taasisi hiyo ya elimu.

Wakazi wa eneo hilo wanahisi kwamba majengo yaliyosalia ya shule hiyo huenda yasidumu muda mrefu bila kuathiriwa na maji.

Shuke nyingine 13 na vituo 33 vya chekechea vimeathiriwa na maji ya mafuriko katika eneo hilo kufuatia mto Tana kuvunja kingo zake kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika sehemu mbali mbali nchini.