Shule kote nchini huenda zikakosa kufunguliwa kwa muhula wa tatu mwezi Septemba mwaka huu, kutokana na mgomo wa walimu.
Vyama vya walimu nchini KNUT na KUPPET vimetishia kutofungua shule iwapo tume ya kuwaajiri walimu ya TSC haitatimiza matakwa yao sita.
Matakwa hayo ni pamoja: kutekeleza kikamilifu makubaliano ya mwaka 2021/2025 kuhusu nyongeza ya mshahara, kupandishwa vyeo kwa walimu 130,000 waliokwama, kuajiriwa kwa walimu vibarua kwa kandarasi za muda mrefu, kusainiwa kwa makubaliano mapya ya nyongeza ya mshahara, kuwasilishwa kwa makato yote ya kuanzia mwaka jana kwa taasisi husika, na kutatua mzozo wa bima ya matibabu kwa walimu.
KNUT na KUPPET wamesimama kidete kuwa iwapo TSC haitasuluhisha matakwa hayo, basi hawatakuwa na budi ila kugoma mwezi Septemba.
Waziri mpya wa Elimu Julius Ogamba anakabiliwa na changamoto ya kutafuta suluhu ya mgomo ambao huenda ukaathiri mitihani ya kitaifa.