Home Habari Kuu Shule, kampuni ya mikopo na eneo la burudani zatozwa faini kwa kutolinda...

Shule, kampuni ya mikopo na eneo la burudani zatozwa faini kwa kutolinda data

0

Afisi ya kamishna wa kulinda data nchini imetoa ilani ya faini kwa shule, kampuni ya mikopo na eneo moja la burudani kwa kutolinda data za wateja.

Kwenye ilani iliyotolewa na ofisi hiyo inayoongozwa na Immaculate Kasait leo Jumanne, mashirika hayo matatu yanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya kulinda data.

Shule ya Roma mtaani Uthiru kaunti ya Nairobi imetozwa faini ya shilingi milioni 4.55 kwa kuchapisha picha za wanafunzi bila idhini ya wazazi wao.

Mkahawa wa Casa Vera kwenye barabara ya Ngong nao umetozwa faini ya shilingi milioni 1.850 kwa kosa sawia. Unadaiwa kukiuka sheria ya kulinda data kwa kuchapisha picha za wateja wake bila idhini.

Kampuni ya Mulla Pride ambayo hutoa mikopo kupitia majukwaa kadhaa kama vile Kecredit na Faircash, imetozwa faini ya milioni 2.975. Inalaumiwa kwa kutumia vibaya nambari za simu zilizohifadhiwa kwenye simu za wateja wake kutuma jumbe za vitisho kwa kukosa kulipa mikopo.

Afisi ya kamishna inachunguza supamaketi ya Naivas na kampuni ya mikopo ya Whitepath baada ya kupokea malalamishi.

Wote ambao hutagusana na data za Wakenya wameonywa wazingatie sheria.

Website | + posts