Shule 338 Kenya zawahudumia wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalum

Martin Mwanje
2 Min Read

Kenya ina shule 338 za msingi na sekondari za umma zinazowahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum na wanaoishi na ulemavu. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Elimu Dkt. Elyas Abdi.

Dkt. Abdi amesema shule 300 za msingi na 38 za sekondari zinawahudumia watoto wanaoishi na ulemavu akiongeza kuwa fokasi ya Kenya kwa elimu ya mahitaji maalum inabadilika. 

Mkurugenzi huyo alitoa kauli hizo alipofungua kongamano juu ya Tukio la Mafunzo ya Ulemavu—Elimu Jumuishi Mashariki na Kusini mwa Afrika: Mafanikio ya Kenya kuhusiana na Elimu Jumuishi ya Ulemavu wakati wa hafla iliyofanyika katika hoteli moja jijini Nairobi. 

Dkt. Abdi alisema serikali inaelekea katika utekelezaji wa elimu jumuishi ambapo watoto wenye ulemavu wanahudhuria shule za kawaida na kurudi nyumbani kwao. 

Kwa upande wake, Mshauri wa Elimu wa Ofisi ya Kikanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESARO) Wongani Taulo, alielezea haja ya kuimarisha mipangokazi ya sera kuhusu mahitaji ya watoto wenye ulemavu. 

Alisema ugavi wa rasilimali kwa elimu ya mahitaji maalum unapaswa kuwa wa usawa kuhakikisha hakuna mtoto anayewachwa nyuma inapokuja kwa masuala ya elimu. 

Aliongeza kuwa kubadikika kwa jamii na walimu katika viwango vya elimu ni muhimu katika kufanikisha elimu ya watoto wenye ulemavu. 

Mkurugenzi wa Elimu ya Mahitaji Maalum Fredrick Haga alisema wakati wa sasa ni wa elimu jumuishi ambapo watoto wenye ulemavu wanapaswa, kadiri iwezekanavyo, kusomea katika shule za kawaida. 

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha watoto wanaoweza kusoma, kusalia na familia zao. 

“Ni watoto wenye ulemavu mkubwa pekee ambao wanapaswa kusomea katika shule zenye mahitaji maalum,” Haga alisema pembezoni mwa kongamano hilo lililovutia washiriki kutoka nchi za Kenya, Malawi, Lesotho, Tanzania bara na Zanzibar. 

Website |  + posts
Share This Article