Home Habari Kuu Shughuli za uchimbaji mchanga zasimamishwa kaunti ya Homa Bay

Shughuli za uchimbaji mchanga zasimamishwa kaunti ya Homa Bay

Maeneo yaliyoathirika yanajumuisha Osodo katika eneo la Karachuonyo, Gem eneo la  Rangwe, Gingo lililoko Suba Kaskazini, na Ogande katika mji wa Homa Bay.

0
Ukusanyaji na uchimbaji mchanga wapigwa marufuku Homa Bay.

Kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa katika maeneo mengi hapa nchini ambayo imesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, shughuli za uchimbaji mchanga katika kaunti ya Homa Bay zimesimamishwa mara moja.

Akitoa agizo hilo, kamishna wa kaunti ya Homa Bay Moses Lilan, alisema hatua hiyo inalenga kuzuia maafa ikizingatiwa hatari iliyoko katika maeneo hayo ya ukusanyaji na uchimbaji mchanga.

Maeneo yaliyoathirika yanajumuisha Osodo katika eneo la Karachuonyo, Gem eneo la  Rangwe, Gingo lililoko Suba Kaskazini, na Ogande katika mji wa Homa Bay.

Lilan alisema mvua inayoendelea kunyesha inadhoofisha udongo katika maeneo hayo na inaweza kusababisha maporomoko ya ardhi.

Alitoa wito kwa wazazi kuwashauri watoto wao kutokucheza karibu na matimbo ili kuepuka maafa yaliyoshuhudiwa katika maeneo hayo hapo awali.

Alikariri kuwa mipango inaendelea ya kuwahamisha waathiriwa wa mafuriko ambao kwa sasa wanaishi shuleni huku wanafunzi wakijiandaa kurejea darasani wiki ijayo.

Website | + posts