Home Habari Kuu KEMSA yatuzwa na shirika la utafiti wa ubora nchini Uingereza

KEMSA yatuzwa na shirika la utafiti wa ubora nchini Uingereza

0

Shirika la kusambaza dawa na vifaa tiba nchini, KEMSA limeiweka Kenya katika ramani ya ulimwengu baada ya kushinda tuzo ya uongozi katika ubora mwaka huu wa 2024.

KEMSA ambayo awali ilikumbwa na kashfa mbalimbali za ufisadi imepewa tuzo hiyo na shirika la utafiti wa ubora ulimwenguni, ESQR nchini Uingereza.

Tuzo hiyo inajiri yapata miezi miwili tangu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Dkt. Andrew Mulwa aliposhinda tuzo ya utawala barani Afrika mwaka 2024, kutokana na juhudu zake za kubadili shirika hilo.

Alitambuliwa kwa kufanya KEMSA kuwa shirika la kipekee la usambazaji wa dawa na vifaa vya matibabu barani Afrika na hafla ya tuzo hizo iliandaliwa nchini Mauritius.

Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika la KEMSA wametambuliwa na ESQR kwa kubadili mifumo ya ubora katika KEMSA, mifumo ambayo imefanya shirika hilo kuwa bora zaidi katika usambazaji wa bidhaa za matibabu.

Kampuni nyingi, mashirika na taasisi zilisailiwa kwa ajili ya tuzo hiyo kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni kama Uingereza, Bara Asia, Amerika, Afrika na Australia.

ESQR hufuatilia uimarishaji wa mifumo, mbinu na miradi ya utafiti ambayo inachangia utamaduni wa mipangilio ya ubora wa hali ya juu linapotoa tuzo hiyo.

Washindi wa mwaka huu waliafikiwa kupitia kwa mfumo wa upigaji kura, utafiti kati ya watumizi wa bidhaa na huduma za mashirika mbalimbali na takwimu za masoko.

Dkt. Mulwa atakwenda kupokea rasmi tuzo hiyo kwa niaba ya KEMSA mwezi Juni mwaka huu jijini Brussels nchini Ubelgiji.

Website | + posts