Home Habari Kuu Siku ya Mashujaa: Waziri Namwamba kukabidhi Uwanja wa Kericho Green Alhamisi

Siku ya Mashujaa: Waziri Namwamba kukabidhi Uwanja wa Kericho Green Alhamisi

0

Ukarabati wa uwanja wa michezo wa Kericho Green umekamilika siku moja kabla ya sherehe za Siku ya Mashujaa kuandaliwa uwanjani hapo. 

Hafla ya ukabidhi wa uwanja huo itafanyika kesho Alhamisi ikiongozwa na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba.

Rais William Ruto ataliongoza taifa kwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa keshokutwa Ijumaa katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serikalini.

Aidha mashujaa wapatao 250 wataenziwa wakati wa maadhimisho hayo ambayo mandhari yake ni upatikanaji wa afya kwa wote.

Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Kitaifa ikiongozwa na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo na Waziri wa Afya Susan Nakhumicha ilizuru uwanja huo jana Jumanne kukagua ikiwa kila kitu kiko shwari kabla ya maadhimisho ya sherehe za Mashujaa.

Akizungumza na wanahabari baada ya ukaguzi huo, Waziri Nakhumicha aliridhika na maandalizi ya kamati hiyo na kuwakaribisha Wakenya wote, hasa wakazi wa kaunti ya Kericho, kuhudhuria sherehe hizo.

Nakhumicha amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sherehe za mwaka huu za Siku ya Mashujaa zinafanikiwa ikizingatiwa mandhari ya mwaka huu ya upatikanaji wa afya kwa wote yako chini ya himaya yake.

Katibu Omollo kwa upande wake alielezea kwamba wameshuhudia mazoezi ya wahusika kadhaa wa sherehe hizo wakiwemo wanajeshi na wasanii na kwamba ana uhakika wako tayari kutumbuiza watakaohudhuria.

 

Website | + posts