Home Biashara Shehena ya pili ya mbolea ya bei nafuu yazinduliwa

Shehena ya pili ya mbolea ya bei nafuu yazinduliwa

0

Waziri wa Kilimo Mithika Linturi amezindua shehena ya pili ya mbolea ya bei nafuu inayolenga wakulima wa majani chai.

Akizungumza wakati wa kuanzisha msafara wa malori ya kusambaza mbolea hiyo kutoka bandari ya Mombasa, Linturi alisema kwamba gunia moja la kilo 50 litauzwa kwa shilingi 2500.

Shehena iliyozinduliwa leo ni zaidi ya tani elfu 45 sawa na magunia laki 9 na waziri Linturi alisema ipo mipango ya kuhakikisha upatikanaji wa magunia milioni 7 ya mbolea mwakani.

Alihakikishia wakulima kwamba wizara yake imejitolea kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima wa mashamba madogo huku ikiwakinga kutokana na bei ghali.

Kutokana na hilo, magunia ya kilo 25 ya mbolea yataletwa.

Mbolea hiyo ya majani chai itapatikana katika vituo vya kuuzia na kununua majani hayo vya halmashauri inayosimamia maendeleo ya zao la majani chai kote nchini.

Wakulima sasa hawatapata gharama ya ziada ya kusafirisha mbolea kutoka kwenye viwanda vya majani chai ambavyo huenda viko mbali ikilinganishwa na vituo vya kupima na kuuza majani chai.

Website | + posts