Home Habari Kuu Shamrashamra za Sikukuu ya Krismasi

Shamrashamra za Sikukuu ya Krismasi

0

Wakenya waliungana na ulimwengu katika kuadhimisha Sikukuu ya Krimasi kwa mbwembwe za aina yake jana Jumatatu. 

Wengi walifurika makanisani kuomba dua kufuatia kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu Kristo siku hiyo huku bustani kama vile ya Uhuru Park jijini Nairobi na maeneo mengine ya burudani yakiteuka kutokana na wingi wa watu.

Ila wengi walilalamikia kupanda kwa gharama ya maisha nchini, hali waliosema iliwalazimu kutosafiri hadi maeneo walikozaliwa kujumuika na familia kuadhimisha siku hiyo kama ilivyo ada.

Katika makazi ya watoto ya Bethel yaliyopo eneo la Londiani, kaunti ya Kericho, watoto walikuwa na kila sababu ya kutabasamu baada ya mbunge wa Kipkelion Mashariki Joseph Cherorot pamoja na familia yake kujumuika nao kusherehekea siku hiyo.

Akiandamana na wahisani wengine, mbunge huyo alitoa mchango wa vyakula, vitau na bidhaa zingine za matumizi kwa watoto katika makazi yao ili kupamba sherehe zao za Sikukuu ya Krismasi.

Cherorot aliahidi kwamba watoto katika makazi hayo watasaidiwa kupitia hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge ili kugharimia karo yao ya shule.

Kadhalika aliahidi kuwatafutia kazi wale ambao wamekamilisha masomo yao.

Aliupongeza usimamizi wa makazi hayo ikiwa ni pamoja na watunzaji wa watoto hao na wafanyakazi wa kujitolea akisema wametekeleza wajibu muhimu wa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.

Katika eneo bunge la Matayos, kaunti ya Busia, watu wanaoishi na ulemavu walikuwa na kila sababu ya kufurahia baada ya kupokea msaada wa chakula kutoka kwa wakfu wa Jeff Okanya. 

Ni mchango ulioweka tabasamu kwenye nyuso za jamaa wa wale wanaoishi na ulemavu baada ya kupata fursa ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi kama watu wengine. I

Wakfu wa Jeff Okanya uliwapa msaada wa chakula kama vile unga, mafuta ya kupikia, chumvi na bidhaa zingine muhimu za matumizi.

Watu wenye ulemavu mara nyingi hupuuzwa na jamii na kwao, sherehe kama za Sikukuu ya Krismasi huwa haziwaletei furaha jinsi ilivyo kwa watu wengine.

Taarifa zaidi kutoka kwa Selyne Wamala na Erick Kiplangat 

Website | + posts