Home Habari Kuu Serikali yazindua mfumo wa kidijitali kufuatilia miradi yake

Serikali yazindua mfumo wa kidijitali kufuatilia miradi yake

Kulingana na katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo, Project BETA, itahakikisha habari kuhusu miradi na mipango ya serikali inatekelezwa kwa wakati na uadilifu.

0
Serikali yabuni kifaa cha kufuatilia miradi yake.

Serikali imezindua mfumo wa kidijitali cha kutoa ripoti na kukadiria miradi ya serikali ya kitaifa kwa jina “Project BETA”.

Mfumo huo mpya utafuatilia utekelezaji, maendeleo na ufanisi wa miradi ya serikali, mipango inayofaa kupewa kipaumbele, maagizo ya Rais na takwimu kutoka pembe zote za nchi kupitia maafisa wa serikali ya kitaifa.

Kulingana na katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo, Project BETA, itahakikisha habari kuhusu miradi na mipango ya serikali inatekelezwa kwa wakati na uadilifu.

Huku akitoa vipakatalishi kwa makamishna wa maeneo na wale wa kaunti katika taasisi ya mafunzo ya serikali Jijini Nairobi, Dkt. Omollo alisema kuanzia sasa miradi itafuatiliwa kwa wakati huku habari zote za miradi ya serikali zikipatikana katika mfumo mmoja.

“Lengo kuu la mfumo wa Project BETA, ni kuwapa uwezo maafisa wetu kusimamia na kushirikisha sera za serikali ya kitaifai,” alisema katibu huyo.

Huku ikizingatiwa kuwa makamishna wa maeneo na wale wa kaunti ndio viongozi wa kamati za usalama, mfumo wa Project BETA utasaidia pakubwa kunakili visa vya uhalifu na kuvifuatilia.

Miongoni mwa miradi ya serikali ambayo itafuatiliwa kupitia project BETA, ni pamoja na usajili wa wakulima kwa mpango wa utoaji mbolea ya gharama nafuu, idadi ya nyumba zilizojengwa kupitia mradi wa nyumba za gharama nafuu, miti iliyopandwa chini ya kampeni ya upanzi wa miti bilioni 15 na waliosajiliwa kupitia mpango wa inua jamii.

Website | + posts