Home Habari Kuu Serikali yatoa shilingi bilioni 16.7 za Mpango wa Inua Jamii

Serikali yatoa shilingi bilioni 16.7 za Mpango wa Inua Jamii

0

Serikali imetoa shilingi bilioni 16.7 kwa zaidi ya watu milioni moja wanaonufaika na Mpango wa Uhamishaji Fedha wa Inua Jamii.

Fedha hizo ni za kipindi cha mwezi Novemba, 2022 hadi Juni, 2023.

Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Alhamisi amesema Wizara ya Fedha imetoa jumla ya shilingi bilioni 16,725,856 zitakazosambazwa kwa watu 1,072,226 watakaonufaika.

Kila atakayenufaika atapokea shilingi elfu 16 na kwamba fedha hizo zitatolewa katika awamu mbili.

Wanufaikaji wa fedha hizo ni pamoja na watoto mayatima na maskini, wazee na watu wanaoishi na ulemavu.

Akielezea kuwa serikali imedhamiria kuwasaidia Wakenya wasiojiweza kifedha, Gachagua alisema fedha hizo zitaongezwa katika bajeti ya ziada ili kuongeza idadi ya wanufaikaji hadi milioni 2.5 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

“Tunaendelea kutekeleza Mpango wa Uhamishaji Fedha unaojulikana mno kama Inua Jamii ambao unatoa fedha kila baada ya miezi miwili ili kuwakinga wanufaikaji dhidi ya umaskini. Hii imelenga kuboresha maisha yao,” alisema Naibu wa Rais.

Aliyasema hayo katika makazi yake rasmi mtaani Karen akiwa ameandamana na maafisa mbalimbali wa serikai wakiongozwa na Waziri wa Leba Frolence Bore.


Gachagua alisema fedha zingine milioni 11,185,000 zitalipwa kama nyongeza kwa wanufaikaji chini ya mpango wa Uboreshaji wa Lishe Kupitia Elimu ya Fedha na Afya (NICHE).

Hii inafanya jumla ya fedha zilizotolewa chini ya mipango hiyo miwili kuwa bilioni 16,737,041,000.

Alisema fedha hizo zitawekwa kwenye akaunti za wanufaikaji.

Kila mnufaikaji atapokea shilingi elfu 16 zitakazolipwa katika awamu mbili ikiwa ni mwezi Juni na Julai, 2023, yakiwa malipo ya vipindi vinne.

Malipo yataanza kutolewa Juni 28, 2023 kupitia benki sita zilizopewa kandarasi na serikali kutekeleza wajibu huo.

Katika kila kipindi, serikali itatoa shilingi bilioni 4,184,260,500.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here