Home Biashara Serikali yatoa ruzuku kwa KCC kununua maziwa ya ziada kutoka kwa wakulima

Serikali yatoa ruzuku kwa KCC kununua maziwa ya ziada kutoka kwa wakulima

0
kra

Serikali imetoa ruzuku kwa kampuni ya kutayarisha maziwa nchini KCC ili iweze kununua maziwa ya ziada kutoka kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Hatua hii inafuatia ongezeko la kiwango cha maziwa yanayozalishwa kutokana na mvua nyingi na upatikanaji wa lishe ya mifugo na lalama za wafugaji za kukosa soko la bidhaa hiyo ambayo sasa inapatikana kwa wingi.

kra

Katika kikao na wanahabari leo, waziri wa vyama vya ushirika Simon Chelughui alielezea kwamba mvua inayonyesha kwa sasa itasababisha uzalishaji wa lita milioni 50 zaidi za maziwa kati ya sasa na mwezi Januari mwakani.

Alisema kwamba iwapo maziwa hayo hayataongezwa thamani yataharibika na hiyo ni hasara kubwa kwa wafugaji.

Kulingana naye mpango wa kununua maziwa hayo kutoka kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa utagharimu shilingi bilioni 1.5 na leo wametoa milioni 500 za kwanza za kuufanikisha.

“Serikali imezingatia kwa makini athari za mvua ya El Nino kwa sekta ya maziwa ndiposa imetoa pesa hizo.” alielezea Chelugui, huku akihakikishia wakulima kwamba serikali inawaunga mkono kikamilifu.

Awali wakulima wanaojihusisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa walikuwa wamelalamikia hasara wanayopata wakisema maziwa ni mengi na wanunuzi ni wachache na bei ni ya chini mno.

Website | + posts