Rais William Ruto ametangaza siku tatu za kitaifa kuwaomboleza wanafunzi 18 wa shule ya Hillside Endarasha Nyeri, waliofariki katika mkasa wa moto.
Kupitia kwa taarifa Rais alisema, “Kwa heshima ya wanafunzi 18 waliofariki ambao watakumbukwa daima katika historia ya Kenya, taifa hili litawaomboleza kwa siku tatu.”
Kiongozi wa taifa aliagiza bendera ya Kenya na ile ya Afrika Mashariki kupeperushwa nusu mlingoti, kama ishara ya maombolezi ya kitaifa na heshima kwa waathiriwa.
Siku hizo tatu za maombolezi zitaanza Jumatatu Septemba 9 na kukamilika Septemba 11, 2024.
Kuhusu wanafunzi waliojeruhiwa wanaopokea matibabu, Rais aliwatakia afueni ya haraka akiahidi kuwasaidia.
“Tunawatakia afueni ya haraka, tunawaombea pamoja na familia zao,” alisema kiongozi wa nchi.
Rais Ruto aliahidi kuhakikisha uwajibikaji katika shule zote kote nchini, akisisitiza kuhusu usalama wa wanafunzi.
Alitoa wito wa umoja na ushirikiano wakati wa kipindi hicho cha maombolezi.