Home Habari Kuu Serikali yatangaza Ijumaa kuwa sikukuu

Serikali yatangaza Ijumaa kuwa sikukuu

0
Rais William Ruto.

Rais William Ruto ametangaza kwamba Ijumaa Mei 10, 2024 ni sikukuu ya kitaifa ambayo imetengwa kwa ajili ya kukumbuka waathiriwa wa mafuriko.

Akizungumza katika ikulu ya Nairobi wakati wa mkutano na viongozi wa eneo la Kajiado ya kati na Laikipia Kaskazini, kiongozi wa nchi alisema kwamba siku hiyo pia itatumiwa kwa upanzi wa miti.

Tangazo hilo limechapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali na kiongozi wa nchi alisema wakenya watakumbuka kwamba suluhisho kwa mabadiliko ya tabianchi ni utunzaji wa mazingira hususan upanzi wa miti.

Waziri wa mazingira Soipan Tuya anatarajiwa kuandaa mkutano na wanahabari kufafanua zaidi kuhusu sikukuu hiyo.

Ni katika kikao cha leo na viongozi hao wa mashinani wakiongozwa na wabunge Kanchory Memusi na Sarah Korere Rais alitangaza ufunguzi wa shule kwa muhula wa pili Jumatatu tarehe 13.

Ufunguzi huo uliahirishwa mara mbili kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha na ambayo ilisababisha mafuriko katika maeneo mbali mbali nchini.

Shule zilikuwa zimepangiwa kufunguliwa Aprili 29, 2024 lakini waziri wa elimu Ezekiel Machogu akaahirisha kwa wiki moja hadi Mei 6, 2024 na baadaye Rais Ruto akaahirisha kwa muda usiojulikana.

Kuhusu ukarabati wa barabara na shule zilizoharibiwa na mafuriko Rais alisema kwamba atashirikisha washirika wa kimaendeleo kuutekeleza na hazina ya ustawi wa maeneo bunge pia itachangia.