Baadhi ya wabunge kutoka kaskazini mwa nchi wameitaka serikali kuu kutangaza mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha katika sehemu mbalimbali za nchi kuwa janga la kitaifa.
Wanasema hali kaskazini mashariki mwa nchi imekuwa mbaya na maji yatazidi unga ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Wakiongozwa na mbunge wa Wajir Kaskazini Ibrahim Saney, wabunge hao wanasema wakazi wa eneo hilo kwa sasa wanakumbwa na uhaba wa chakula huku kukiwa na uwezekano wa kutokea kwa mlipuko wa magonjwa.
Ingawa wanasema Mawaziri Prof. Kithure Kindiki wa Usalama wa Kitaifa na Aden Duale wa Ulinzi wamejizatiti kutoa msaada wa chakula kwa wakazi, kuna haja ya juhudi hizo kuongezwa maradufu.
Kulingana nao, msaada uliotolewa kufikia sasa ni tone la maji lisiloweza kukata kiu.
Kauli zao zikiwadia wakati kaunti ya Mandera inahangaika kutokana na athari za mvua kubwa ambayo imesababisha mafuriko, vifo na uharibifu mkubwa.
Barabara kuu katika mji wa Mandera Mashariki zimefunikwa na mafuriko huku baadhi ya barabara zikiwa hazipitiki kabisa.
Wasiwasi wa kutokea kwa uhaba wa chakula na kupanda kwa gharama ya maisha unaongezeka wakati wakazi wakikabiliwa na uhaba wa bidhaa muhimu.
Wakazi wanahofia kutokuwepo kwa bidhaa zinazoingizwa katika kaunti hiyo.
Kulingana na Abd Adow ambaye ni mkazi wa kaunti hiyo, janga linakodolea macho ikiwa hali hiyo itaendelea.
Kufungwa kwa masoko makuu ambayo hutumiwa na zaidi ya wakazi 200,000 wa Mandera Mashariki kumezidisha hali kuwa mbaya na kufanya eneo hilo kutofikika.
Bidhaa muhimu kama vile mboga zimeisha na kufanyaa mfumko wa bei katika kaunti hiyo kufikia viwango visivyowahi kushuhudiwa.
Bei za bidhaa muhimu kama vile sukari, mchele na mboga nazo zimepanda kwa shilingi 2,200.
Mohamed Hussein, mkazi mwenye mashaka mengi, anatoa wito kwa serikali na viongozi wa eneo hilo kuingilia kati kwa dharura kabla ya mambo kwenda mrama zaidi.
Ujumbe sawia unatolewa na Naibu Gavana Ali Maalim anayeonya kuwa bila hatua kuchukuliwa haraka, hali hiyo itashindwa kudhibitiwa.
Katika kipindi cha saa 48 zilizopita, kaunti ya Mandera imeshuhudia mvua kubwa ambayo imesababisha wakazi 39,000 kupoteza makazi na uharibifu wa nyumba zaidi ya 8,000.