Home Habari Kuu Serikali yasitisha ada mpya kutoa nafasi kwa ushirikishi wa umma

Serikali yasitisha ada mpya kutoa nafasi kwa ushirikishi wa umma

0
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki

Wakenya wamepata afueni ya muda baada ya serikali kutangaza kusitishwa kwa utekelezaji wa ada mpya za huduma mbali mbali za serikali.

Kwenye taarifa kwa umma waziri wa mambo ya ndani Profesa Kithure Kindiki amesema kwamba ada hizo alizotangaza kupitia machapisho nambari 15239, 15240, 15241 na 15242 ya mwaka 2023 ya gazeti rasmi la serikali toleo la 239 la Novemba 7, 2023, zimesitishwa.

Sasa waziri Kindiki amependekeza viwango tofauti vya ada hizo na kutoa fursa kwa wakenya kutoa maoni yao. Iwapo zitakubalika, ada hizo zitaanza kutekelezwa Januari 1, 2024.

Ameelekeza idara ya uhamiaji kutekeleza shughuli ya ushirikishi wa umma kuhusu ada hizo haraka iwezekenavyo na iwe imekamilika kufikia Disemba 10, 2023.

Kindiki ametetea ada hizo akisema zinanuiwa kusaidia Kenya kujitegemea kifedha na kuacha kutegemea mikopo ya kigeni ambayo haiwezi kumudu.

Kulingana naye wakenya ambao watakuwa wanatafuta vitambulisho kwa mara ya kwanza na ambao watadhihirisha kwamba hawataweza kulipia stakabadhi hiyo wataondolewa ada.

Wakenya walikuwa wamelalamika kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ada mpya zilizopendekezwa ikiwa ni pamoja na ada ya kupata kitambulisho iwapo kimepotea.

Awali stakabadhi hiyo ilikuwa ikilipiwa shilingi 100 na serikali ikapendekeza kuongeza hadi shilingi 2000.

Ada za paspoti za usafiri pia zilikuwa zimeongezwa maradufu.

Website | + posts