Home Habari Kuu Serikali yasimamisha ukusanyaji data wa WorldCoin

Serikali yasimamisha ukusanyaji data wa WorldCoin

0

Serikali kupitia wizara ya mambo ya ndani imesimamisha mipango ya ukusanyaji data ya watu binafsi ambao unaendeshwa na kampuni ya World Coin na kampuni nyingine ambazo zinaendesha mipango sawia.

Kwenye taarifa ya Agosti 2, 2023, wizara hiyo inatilia shaka usalama wa data ya wakenya ambao wamekuwa wakipanga foleni ndefu kwenye vituo mbali mbali vya kibiashara kusomwa na kunakiliwa macho na kisha kupatiwa sarafu za worldcoin ambazo thamani yake ni sawa na shilingi elfu 7.7 za Kenya.

Taarifa hiyo inasema kwamba mashirika kadhaa ambayo ni ya usalama, huduma za kifedha na ulinzi wa data yameanzisha uchunguzi kubaini uhalisia na uhalali wa mpango huo. Wahusika wanatafuta kujua usalama wa data inayokusanywa na jinsi itatumika.

Waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki amesema kwamba serikali itachukua hatua zifaazo kuhakikisha usalama na uadilifu wa mipango yote ya kifedha inayohusisha idadi kubwa ya wakenya.

Alisema pia kwamba yeyote ambaye atasaidia kuendeleza mipango hiyo wakati huu ambapo imesimamishwa atachukuliwa hatua za kisheria.

Hatua hii inajiri baada ya waziri wa teknolojia ya mawasiliano na uchumi digitali Eliud Owalo kusema kwamba serikali haikuwa imechukua hatua dhidi ya kampuni hiyo ya Worldcoin kwa sababu haikuwa imekiuka sheria.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga, waziri Owalo hata hivyo alithibitisha kwamba serikali ilikuwa inachunguza WorldCoin ili kuelewa shughuli zake na mipango yake ya kulinda data.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here