Home Habari Kuu Serikali yaorodhesha mipango ya kukabiliana na athari za El Nino

Serikali yaorodhesha mipango ya kukabiliana na athari za El Nino

0

Rais William Ruto aliandaa kikao cha baraza la mawaziri leo asubuhi kwa nia ya kutafuta njia za kukabialana na athari za mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini.

Katika kikao hicho mipango kadhaa iliorodheshwa ya kusaidia watu wa maeneo ambayo yameathiriwa na mvua hiyo ambazo ni kaunti 38.

Iliarifiwa kwamba baraza la mawaziri lilitenga shilingi bilioni 7 za kukabiliana na athari hizo ambazo zitatumika kusaidia wakulima walioathirika.

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa ndio wamefaidika zaidi ambapo shilingi milioni 500 zimetengewa kampuni ya KCC ili iweze kununua maziwa kutoka kwao.

Chakula cha msaada cha thamani ya shilingi milioni 180 kitanunuliwa na kusafirishwa kwa ndege za jeshi la KDF hadi kaunti ya Wajir.

Baraza hilo la mawaziri lilielekeza pia kwamba ndege za KDF na nyingine za kampuni za usafiri zitumiwe ipasavyo kusafirisha misaada ya chakula, dawa na vifaa vingine hadi maeneo ambayo yameathirika.

Kuhusu ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua, serikali iliorodhesha ile ambayo inahitaji kurekebishwa haraka kama vile daraja la Mbogolo katika barabara kuu ya kutoka Mtwapa kuelekea malindi.

Uwanja mdogo wa ndege wa Garissa tayari umekarabatiwa na shughuli humo zitarejelewa keso.

Wizara ya fedha ilielekezwa itoe fedha zingine bilioni 10 kwa serikali za kaunti wiki hii ili ziweze kukabiliana na athari za mvua na mafuriko.

Walipendekeza pia kwamba pendekezo liwasilishwe bungeni la kuongeza pesa katika hazina ya dharura na bunge liratibishe bajeti hiyo chini ya mswada wa pili wa bajeti ya ziada ya mwaka 2023/24.

Wizara ya kawi ilielekezwa itoe kipaumbele kwa utengenezaji wa nguvu za umeme kutoka kwa maji ambayo sasa ni mengi na itangulie kusambaza umeme huo.

Kando na hilo wizara hiyo ilielekezwa kuhakikisha kwamba wateja wa umeme wanafurahikia bei iliyopunguzwa ya nguvu za umeme zinazotokana na maji.

Website | + posts