Home Burudani Kodi ya kuwaongezea wasanii mapato kutozwa kuanzia Septemba 15

Kodi ya kuwaongezea wasanii mapato kutozwa kuanzia Septemba 15

0
kra

Serikali itaanza kuzitoza kodi kanda za kunasia sauti, kodi inayojulikana kama “Blank Tape Levy” kuanzia Septemba 15, 2023.

Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki ya Mwaka 2001.

kra

Kodi hiyo itatozwa kwenye vifaa vyote vinavyoweza kutumika kurekodi au kubeba maudhui yaliyolindwa na hakimiliki, na malipo yatafanyika katika vituo vya kuingilia nchini Kenya.

Kodi ya “Blank Tape Levy” inalenga kulinda hakimiliki za wasanii na mali miliki ya raia wa Kenya.

Sheria hii itaanza kutekelezwa baada ya marekebisho na mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Waziri wa Michezo Ababu Namwamba na wadau wa sekta ya burudani.

Aidha inalenga pia kukusanya mapato yatakayosaidia kuendeleza sekta ya sanaa nchini.

Baadhi ya vifaa vinavyoathiriwa na kodi hii ni pamoja na vifaa vya kurekodia, na simu za mkononi. Aidha, televisheni, redio, simu za mkononi, vifaa vya USB, CD, na DVD vitatozwa kodi hii.

Kodi hii itaathiri bei za vifaa hivi, kwani kodi itaongezwa kwenye bei ya vifaa vyote vyenye uwezo wa kutumika kwa madhumuni ya kibinafsi.

Akizungumza Na KBC, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hakimiliki za Muziki Nchini, MCSK Ezekiel Mutua, amehakikisha kuwa ingawa hii inaweza kusababisha bei kupanda kidogo, itasaidia kuongeza mapato ya wasanii na kuendeleza sekta ya sanaa nchini.

Serikali inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 6 kutokana na kodi hiyo. Hii ni sehemu ya jitihada za serikali za kukuza sekta ya ubunifu na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya sanaa.

Kodi hii inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Bodi ya Hakimiliki ya Kenya, Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA), KenTrade, na wadau wengine wa sekta ya hakimiliki.

Gene Gituku
+ posts