Home Habari Kuu Serikali yakarabati barabara ya Marala-Baragoi kukabiliana na utovu wa usalama

Serikali yakarabati barabara ya Marala-Baragoi kukabiliana na utovu wa usalama

Murkomen alibainisha kuwa watu kadhaa wamefariki baada ya kupigwa risasi na majambazi wanaotumia fursa ya hali mbaya ya barabara kutekeleza mashambulizi.

0
Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen akagua ujenzi wa barabara yaMaralal-Baragoi.

Katika juhudi za kukabiliana na utovu wa usalama katika kaunti ya Samburu, serikali imeanzisha ukarabatiwa wa barabara ya Maralal-Baragoi ambayo ni ya urefu wa kilomita 100.

Akiongea alipozindua ukarabati wa barabara hiyo katika eneo la Morijo, waziri wa uchukuzi na miundo msingi Kipchumba Murkomen, alisema ukarabati huo utawezesha wafugaji kupata masoko ya mifugo yao na maafisa wa usalama kujibu haraka mashambulizi ya majambazi na wezi wa mifugo yanapotokea.

“Juhudi tunazotekeleza kuimarisha miundomsingi, zitapiga jeki jitihada za wizara ya usalama wa taifa katika kukabiliana na ujangili na wizi wa mifugo katika kaunti ya Samburu….shughuli hii itatekelezwa hadi katika mpaka wa Kenya na Ethiopia,”

Murkomen alibainisha kuwa watu kadhaa wamefariki baada ya kupigwa risasi na majambazi wanaotumia fursa ya hali mbaya ya barabara kutekeleza mashambulizi.

Waziri huyo alisema wizara hiyo kupitia halmashauri ya kitaifa ya usimamizi wa barabara kuu hapa nchini-KeNHA  imetumia shilingi milioni 50 kuboresha barabara hiyo ya kiwango cha A4 ambayo kwa miaka mingi imekuwa haijakuwa ikipokea kiasi cha kutosha cha ukarabati.

Murkomen pia alifichua kuwa juhudi za kupata ufadhili wa uwekaji lami barabara ya Maralal-Baragoi-Sarima kuelekea Ilerate ya kilomita 400 ziko katika hatua za mwisho mwisho.