Home Kimataifa Serikali yakanusha madai ya kuzuka upya kwa COVID-19

Serikali yakanusha madai ya kuzuka upya kwa COVID-19

Dkt. Amoth alisema wizara imekuwa ikifuatilia visa hivyo kwa kubuni mfumo maalum wa kubaini uwepo wake.

0
Kaimu mkurugenzi wa afya Dkt. Patrick Amoth.

Wizara ya Afya imekanusha madai kuwa maradhi ya kupumua yanayoshuhudiwa nchini yamechangiwa na kurejea kwa virusi vya korona (COVID-19).

Kupitia kwa taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, Wizara hiyo imesema hali hiyo imetokana na mafua ya kawaida.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya Dkt. Patrick Amoth amesema visa vya mafua huwa vinaongezeka sana kati ya mwezi Februari na Machi na Julai hadi Novemba.

“Hakuna visa vyovyote vya COVID-19 ambavyo vimeripotiwa. Kile kimeripotiwa ni ongezeko la visa vya mafua ya kawaida,” alisema Dkt. Amoth.

Hata hivyo, Dkt. Amoth alifichua kuwa wanafuatilia uwezekano wowote wa kurejea kwa virusi vipya vya korona aina ya JNI tangu Novemba 2023.

Aliongeza kuwa wizara imekuwa ikifuatilia visa hivyo kwa kubuni mfumo maalum wa kubaini uwepo wake.

Aliwaagiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka kutangamana na watu wanaoonyesha dalili za maradhi ya kupumua, kupata chanjo dhidi ya aina za mafua, kutumia barakoa katika maeneo ya umma na kunawa mikono kwa sabuni.

Dkt. Amoth aliondoa hofu kuwa mafua hayo ni makali akisema kuwa Wakenya wanaweza kujitibu bila kuenda hospitalini.

Hata ingawa mafua hayo si makali, yanaweza kusababisha kifo kwa watu walio na matatizo ya kiafya.

Wizara ya Afya imetoa taarifa hiyo wiki moja baada ya madaktari nchini kuelezea hofu kuhusu ongezeko la maradhi ya kupumua nchini.

Madaktari hao wamehusisha hali hiyo na kurejea kwa maradhi ya COVID-19.

Alphas Lagat
+ posts