Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani ameitaka serikali ya kitaifa kuongeza mgao wa fedha za kaunti ili kutatua migomo ya mara Kwa mara ya wahudumu wa afya kote nchini.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya wauguzi na wakunga katika zahanati ya Mvindeni wadi ya Ukunda eneo bunge la Msambweni, Achani amelitaka bunge ya Seneti na lile la Kitaifa kuhakikisha kuwa kaunti zinapata mgao wa kutosha ili kutoa huduma tajika katika kaunti.
Achani aliyeshiriki matembezi na wauguzi, alisema tangu ugatuzi ulipoanza sekta ya afya imeboreka katika kaunti ya Kwale kutokana na ujenzi wa vituo zaidi vya afya kutoka 138 hadi 159.
Alitaja pia kuajiriwa kwa wahudumu zaidi wa afya kutoka 600 Hadi 1800 hali ambayo imewaondolea wakaazi wa Kwale dhiki ya kutafuta matibabu.
Achani alipuzilia mbali tetesi za baadhi ya wadau za kutaka usimamizi wa sekta ya afya kurejeshwa kwa serikali ya kitaifa na akisema sekta hiyo imeboreka zaidi ikilinganishwa na wakati wa kabla ya ugatuzi.
Kwa upande wao Diana Joto na Trizah Ireri ambao ni wakuu wa wauguzi katika jimbo la Kwale wamepongeza serikali ya kaunti kwa kuwahakikishia Mazingira bora ya kikazi.
Walisema kuboreshwa Kwa sekta ya Afya katika kaunti ya Kwale kumebuni nafasi zaidi za ajira kwa wahudumu wa afya na wamewezeshwa kuendeleza masomo yao.