Home Habari Kuu Walimu wahakikishiwa usalama maeneo yanayokumbwa na wizi wa mifugo

Walimu wahakikishiwa usalama maeneo yanayokumbwa na wizi wa mifugo

0

Serikali imetoa hakikisho la usalama kwa walimu wanaohudumu katika maeneo yanayokumbwa na wizi wa mifugo eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Akizingumza katika shule ya upili ya Henry Kosgei Kibukwo huko Tinderet, kaunti ya Nandi, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alisema jukumu kubwa la serikali ni kuhakikisha usalama kwa wananchi na mali hivyo basi juhudi zote zimewekwa kuhakikisha usalama wa walimu na wanafunzi katika maeneo yanayokumbwa na uwizi wa mifugo.

Machogu alisema ingawa mashambulizi kadhaa yameripotiwa katika kaunti ya Baringo, wizara hiyo haijafunga shule yoyote.

Aliongeza kuwa wizara yake inashirikiana na Wizara ya Usalama wa Kitaifa kuhakikisha usalama thabiti katika maeneo hayo.

Waziri huyo alisema kuwa Wizara ya Usalama wa Kitaifa kwa ushirikiano wa Wakurugenzi wa Elimu katika kaunti na kaunti ndogo iko mbioni kutathmini hali ili kuwezesha Wizara ya Elimu kuchukua hatua za kuimarisha elimu katika maeneo yaliyoathiriwa.

“Tunafahamu kuwa kutokana na hofu, baadhi ya walimu na wanafunzi hawaendi shule. Hata hivyo, tunashirikiana na Wizara ya Usalama kutathmini hali kabla ya kutangaza kuwa tumefunga shule yoyote iliyoathiriwa”.

Aidha, Machogu alitoa wito wa utulivu akisema wizara inadhibiti hali hiyo na itatoa taarifa ya kina hivi karibuni mara tu tathmini inayoendelea itakapokamilika.

Viongozi wengine waliokuwepo katika hafla hiyo ni mbunge wa Tinderet Julius Melly, mbunge wa Emgwen Josses Lelmengit na Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Tinderet Esther Oyugi miongoni mwa wengine.

Melly ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu Elimu alisema usalama wa walimu katika maeneo yaliyokumbwa na wizi wa mifugo ni jambo linalopaswa kutiliwa maanani.

Aliongeza kuwa kamati hiyo imeandika barua kwa Waziri wa Usalama Prof. Kithure Kindiki ikimwomba kutoa maelezo kuhusu hali ya maeneo yaliyokumbwa na wizi wa mifugo.

“Tunasubiri ripoti ya Waziri wa Usalama ili kamati iweze kuijadili na kutoa mapendekezo,” alisema Melly.