Home Habari Kuu Serikali yachapisha majina ya washukiwa wa ugaidi Lamu

Serikali yachapisha majina ya washukiwa wa ugaidi Lamu

0

Serikali ya Kenya imechapisha majina na picha za washukiwa wa ugaidi, wanaoaminika kuhusika katika mashambulizi ya hivi punde katika kaunti ya Lamu.

Idara ya upelelezi wa jinai, DCI imewaagiza washukiwa hao kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi mara moja.

Miongoni mwa washukiwa hao 35, kunao raia wa Tanzania, Somalia, raia mmoja wa Ujerumani, mmoja wa Uingereza, mmoja wa Bangladesh huku wengine wakiwa raia wa Kenya.

Kulingana na DCI, washukiwa hao wamehusishwa na kuweka vilipuzi katika barabara kadhaa na mauaji ya raia katika barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Vile vile, wanahushishwa na shambulizi lililotekelezwa katika kambi ya kijeshi ya Marekani ya Manda mwaka 2020.

Washukiwa hao wametajwa na Wizara ya Usalama wa Taifa kuwa hatari na waliojihami, na kwamba wao ni sehemu ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab ambalo limetekeleza mashambulizi katika kaunti ya Lamu na msitu wa Boni.

Mamlaka zinasema “tuzo kubwa” itakabidhiwa yeyote atakayetoa taarifa zinazosaidia katika kumkamata mshukiwa yeyote.

“Kitita kikubwa cha fedha kitatolewa kwa raia yeyote atakayetoa taarifa za kuaminika zitakazosaidia katika kumkamata mshukiwa yeyote. Taarifa kuwahusu washukiwa zinapaswa kutolewa kisiri kwa nambari ya moja kwa moja ya 0800 722 203 au 999,” ilisema DCI katika taarifa.

Wanamgamo wa Al-Shabaab wamezidisha mashambaulizi kaskazini mashariki mwa Kenya na katika maeneo ya pwani katika miezi ya hivi karibuni.

Wanamgambo hao wenye uhusiano na kundi la al-Qaeda wanakabiliwa na msako mkali kutoka kwa serikali ya Somalia inayotaka kuwafurusha nchini humo.

Website | + posts