Home Habari Kuu Serikali yabuni sekretarieti ya kupigia debe uenyekiti wa Raila AUC

Serikali yabuni sekretarieti ya kupigia debe uenyekiti wa Raila AUC

0

Waziri mwenye Mamlaka Makuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amezindua kampeni ya serikali ambayo itapigia debe uwaniaji wa Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa  Afrika, AUC.

Mudavadi alidokeza kuwa serikali imebuni sekretarieti inayojumuisha wataalam na wapangaji mikakati kuongoza azima ya Raila kuwania wadhifa huo.

Katika mkutano adimu wa pamoja na wanahabri leo Jumatano jijini Nairobi, Mudavadi alisema Raila ni kiongozi aliye na maono, ambaye atapandisha hadhi ya bara la Afrika

Alielezea kuwa Raila ana tajiriba ambayo inawiana na maadili ya AUC.

Huku akimshukuru Rais Ruto kwa kuidhinisha uwaniaji wa Raila kuwa mwenyekiti wa AUC, Mudavadi alisema hadi kufikia sasa, uwaniaji huo umepokelewa vyema.

“Ninamshukuru Rais William Ruto kwa kumuidhinisha kikamilifu Raila Odinga na pia kwa kuendelea kujadiliana na marais wenzake wa bara hili,” alisema Mudavadi.

Kulingana na Waziri huyo wa Mambo ya Nje, sekretarieti hiyo  iliyobuniwa inajumuisha maafisa wa serikali pamoja na kundi kutoka upande wa Raila na inatarajiwa kuimarisha kampeni za Raila.

Kwa upande wake, Raila alipongeza juhudi zinazotekelezwa na serikali kuunga mkono azima yake ya kuwa mwenyekiti mpya  wa AUC.

“Nimeshauriana na serikali kuhusu jinsi nimejiandaa. Ninafanya bidii kupitia tajiriba yangu, uhusiano na jinsi ninavyoelewa mataifa mengi ya Afrika. Kupitia ushirikiano bora, nina hakika nitatwaa wadhifa huo,” alisema Raila.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alisema anaamini ana uwezo wa kuongoza AUC iwapo atapewa fursa hiyo.

Mnamo Machi 15, 2023, AU ilisema inaunga mkono uwaniaji wa mwenyekiti wa AUC kutoka Afrika Mashariki.

Wadhifa huo kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki Mahamat ambaye ni Raia wa Chad. Muhula wake utakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Website | + posts