Home Habari Kuu Serikali yaagiza kufungwa kwa shule za kutwa Nairobi na Mombasa

Serikali yaagiza kufungwa kwa shule za kutwa Nairobi na Mombasa

0

Seikali imeagiza kufungwa kwa shule zote za msingi na sekondari za kutwa katika kaunti za Nairobi na Mombasa.

Agizo hilo linakuja kabla ya kufanyika kwa maandamano ya siku tatu yaliyopangwa kufanywa na muungano wa upinzani, Azimio kuanzia kesho Jumatano.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Jumanne, Mawaziri Prof. Kithure Kindiki wa Usalama wa Taifa na Ezekiel Machogu wa Elimu walisema shule hizo zitasalia kufungwa kesho Jumatano kama hatua ya tahadhari kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

Taarifa hiyo iliashiria kuwa serikali imepokea taarifa za kuaminika za kijasusi kuwa wahalifu wanapanga kuzua vurugu dhidi ya umma wakati wa maandamano hayo.

“Serikali imepokea taarifa za kiusalama za kijasusi kwamba wahalifu wanapanga kuzua vurugu dhidi ya umma kesho na kukabiliana na maafisa wa usalama karibu na shule fulani ndani ya kaunti za Nairobi na Mombasa,” walisema mawaziri Kindiki na Machogu.

“Kama hatua ya tahadhari ya kuhakikisha usalama wa wanafunzi, imeamuliwa kuwa shule zote za msingi na sekondari za kutwa ndani ya kaunti za Nairobi na Mombasa zisalie kufungwa kesho Jumatano.”

Wizara ya Elimu itatangaza ni lini shule hizo zitafunguliwa tena baada ya kutathmini hali ya usalama hapo kesho.

 

 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here