Home Kaunti Serikali ya kaunti ya Nyandarua kuboresha vivutio vya utalii

Serikali ya kaunti ya Nyandarua kuboresha vivutio vya utalii

Gavana Kiarie Badilisha akikata utepe katika shamba la miti la Olkalou

Ulimwengu unapoadhimisha siku ya kimataifa ya utalii mandhari yakiwa utalii na uwekezaji wa kijani, serikali ya kaunti ya Nyandarua iliadhimisha siku hiyo kwa kuzindua mpango wa makhsusi wa kuboresha shamba la miti la Nyandarua ambao utahakikisha linafanywa kuwa la kisasa na linaafikia viwango vya kimataifa.

Siku ya kimataifa ya utalii huadhimishwa Septemba 27 kila mwaka, tangu mwaka  1970.

Akizungumza katika hafla hiyo katika shamba hilo mjini Olkalou, Gavana Kiarie Badilisha alisema kwamba hata ingawa kuna vivutio vingine vingi vya utalii katika kaunti ya Nyandarua, vingine havijulikani ndiposa watalii hawavizuru kwa wingi.

Badilisha kupitia uongozi wake ameahidi kuanzisha mfumo wa kukuza utalii kwa kuhakikisha maeneo ya utalii yanalindwa yasiingiliwe na binadamu.

Kaunti ya Nyandarua ina maeneo kama mapango yaliyotumiwa na wapiganaji wa Mau Mau, Ziwa Olobolasat, bonde la HAPPY valley na vilima vya Aberdare. Badilisha, anaamini maeneo hayo yakitumiwa vyema yataongeza mapato yanayokusanywa na kubuni nafasi za ajira.

Ili kuafikia hayo, Gavana Badilisha ameahidi kukarabati ziwa Olobolasat ambalo liko katika hatari ya kupotea kutokana na ukame na shughuli za binadamu.

Alisema pia kwamba ushirikiano unahitajika kati ya mashirika husika ambayo ni shirika la huduma kwa wanyamapori KWS, shirika la huduma za misitu KFS, wizara ya ardhi na serikali ya kaunti katika kukabiliana na hatua zozote za binadamu kuvamia maeneo asilia.

Website | + posts
Lydia Mwangi
+ posts