Home Habari Kuu Serikali kuwatuma wakufunzi 1,300 katika taasisi za TVET mwezi Septemba

Serikali kuwatuma wakufunzi 1,300 katika taasisi za TVET mwezi Septemba

0
Katibu katika idara ya mafunzo ya kiufundi Dkt. Esther Muoria.

Wizara ya elimu inalenga kuwatuma wakufunzi 1,300 wa taasisi za mafunzo ya kiufundi(TVET) kote nchini mwezi Septemba mwaka huu.

Katibu katika idara ya mafunzo ya kiufundi Dkt. Esther Muoria, alisema zoezi la kuwaajiri wakufunzi limekamilika na wizara ya elimu inasubiri ripoti ya mwisho kutoka kwa tume ya kuwaajiri watumishi wa umma PSC, kabla ya kuwatuma wakufunzi hao.

Dkt. Muoria aliyasema hayo Ijumaa alipokua akiongoza hafla ya ufunguzi ya mafunzo ya wiki moja kwa wakuu wa taasisi za kiufundi katika kaunti ya Kisumu.

Tume ya kuwaajiri watumishi wa umma, ilitangaza nafasi za wakufunzi wa taasisi za kiufundi TVET mwezi Machi mwaka huu, huku waliotakiwa kutuma maombi wakitakiwa kuwa na shahada, stashahada ya kitaifa au stashahada katika taasisi 220 kote nchini.

Wakati huo huo, katibu huyo alisisitiza haja ya kuwapa mafunzo upya wasimamizi wa taasisi za TVET kuhusu usimamizi wa kifedha, ambao ni nguzo muhimu katika kuboresha taasisi hizo siku za usoni.

“Katika miaka iliyopita, wizara ya elimu imetoa mafunzo kwa maafisa 1,896, ambayo ni asilimia 60 ya idadi inayolengwa,” alisema Muoria.

Website | + posts