Home Habari Kuu Serikali kuwaadhibu vikali wanaodhulumu watoto kimapenzi

Serikali kuwaadhibu vikali wanaodhulumu watoto kimapenzi

Wafula aliwahakikishia wananchi kwamba serikali inamwinda mwanamume ambaye aliahidi kufadhili elimu ya msichana ili kumdhulumu kimapenzi.

0

Kamishna wa kaunti ya Makueni Henry Wafula ameonya kuwa wanaume watakaopatikana wakiwadhulumu wanawake na watoto watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza jana Alhamisi baada ya kufanya mkutano na maafisa wa utawala wa taifa (NGAO) mjini Kibwezi, Wafula alitoa wito kwa wakazi kuripoti visa vyote vya dhuluma za kijinsia na ubakaji ili kusaidia serikali kuwatia nguvuni washukiwa kwa minajili ya kukabiliwa kisheria.

Aidha, aliwarai viongozi wa nyanjani kutekeleza sera za serikali kwa kukabiliana na maovu hayo yanayofanyiwa wanawake na watoto katika kaunti hiyo.

“Hatutakubali watoto wenye umri wa miaka sita kunajisiwa na mtu mzima. Tutawashughulikia wakosaji kwa mujibu wa sheria ya nchi,” alionya Wafula.

Aliwahakikishia wananchi kwamba serikali inamwinda mwanamume ambaye aliahidi kufadhili elimu ya msichana ili kumdhulumu kimapenzi.

“Kuna mtu ambaye amemdhulumu mtoto mdogo kimapenzi, atakimbia lakini hatakuwa na pa kujificha,” aliahidi Wafula.

Kuhusiana na suala la mihadarati, kamishna huyo alisema serikali iko tayari kukabiliana na uovu huo ili kuhakikisha kuwa vijana hawaathiriki vibaya katika jamii.

Mnamo siku ya Jumanne wiki hii, mwakilishi wa kina mama wa kaunti ya Makueni Rose Museo aliwaongoza mamia ya wanawake katika maandamano ya amani mjini Kibwezi kulalamikia kuongezeka kwa dhuluma za kijinsia na ubakaji katika kaunti hiyo.

Alphas Lagat
+ posts