Home Habari Kuu Serikali kusaidia kanisa la Akorino linapoanzisha vyama vya akiba na mikopo

Serikali kusaidia kanisa la Akorino linapoanzisha vyama vya akiba na mikopo

0

Rais William Ruto amesema kwamba serikali ya kitaifa itashirikiana na usimamizi wa kanisa la Akorino nchini katika kutoa mafunzo na uwezeshaji wa aina nyingine, kanisa hilo linapoanzisha mpango wa uwekezaji kwa waumini wake.

Akizungumza alipokutana na viongozi wa kanisa hilo katika ikulu ya Nairobi, Rais alisema kwamba mashirika ya kidini yanaendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya kitaifa.

Kati ya masuala mengine, kiongozi wa nchi alisema mashirika ya kidini yanapiga jeki sekta kama elimu na afya.

Kanisa la Akorino limeanzisha vyama vya akiba na mikopo kwa ajili ya waumini wake kote nchini ndiposa kiongozi wa nchi ameahidi kuunga mkono mipango hiyo.

Mbunge wa Runyenjes Muchangi Karemba muumini wa kanisa hilo na Askofu Petro Kamuyu, mwenyekiti wa kitaifa wa shirika la kidini la Akorino Israel ndio waliongoza ujumbe huo hadi Ikulu.

Kanisa la Akorino ambalo waumini wake hutambulika kwa mavazi ya kipekee hasa kilemba ambacho huvaliwa na wanaume na wanawake lilianzishwa mwaka 1926 katika eneo la kati mwa nchi.