Home Habari Kuu Serikali kusaidia familia ya Kiptum kumwandalia mazishi stahiki

Serikali kusaidia familia ya Kiptum kumwandalia mazishi stahiki

0

Serikali itasaidia familia ya marehemu mwanariadha Kelvin Kiptum kumwandalia mazishi stahiki kama njia ya kutoa heshima kwa shujaa huyo wa kitaifa.

Haya yamesemwa kwenye taarifa kutoka kwa Baraza la Mawaziri ambalo lilifanya mkutano wake leo Jumatano chini ya uenyekiti wa Rais William Ruto.

Kulingana na mawaziri, marehemu Kiptum alikuwa mwanamichezo bora ambaye ufanisi wake katika riadha uliwamotisha wengi kote ulimwenguni.

Anasalia kuwa mtu wa kwanza ulimwenguni kukamilisha marathoni katika muda wa chini ya saa mbili na dakika moja.

Kiptum alikamilisha mbio hizo katika muda wa saa mbili na sekunde 35 na kuweka rekodi mpya ya ulimwengu mnamo Oktoba 8, 2023.

Ushindi huo ulisababisha apate tuzo kadhaa ikiwemo tuzo ya kitaifa ya “the Order of the Grand Warrior – OGW”.

Kelvin Kiptum na kocha wake Garvais Hakizimana waliangamia kwenye ajali ya barabarani usiku wa tarehe 11 Februari mwaka huu wa 2024.

Wizara ya Michezo inaendeleza juhudi za kuhakikisha usalama wa wanamichezo nyota wa kitaifa huku ikihimiza wote kuzingatia usalama barabarani kwa kufuata kanuni zote.

Website | + posts