Wakazi wa eneo bunge la Lari, wamepongeza hatua ya serikali ya kurejelea ujenzi wa barabara ya kilomita 80 ya Mau Mau.
Ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha kaunti za Kiambu, Murang’a, Nyeri na Nyandarua, ulisitishwa kutokana na changamoto za kifedha.
Akizungumza alipozuru mradi huo uliokwama, mbunge wa Limuru Mburu Kahangara aliyekuwa ameandamana na afisa wa kaunti ya Kiambu anayesimamia barabara mhandisi Joseph Mbugua, alisema serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka huu, kukamilisha mradi huo.
Kahangara alidokeza kuwa kukamilishwa kwa barabara hiyo, kutawanufaisha wakazi wa Lari, akiongeza kuwa eneo hilo halipitiki kutokana na miundo msingi mbovu.
Aidha mhandisi Mbugua alisema mradi huo utafungua eneo hilo kimaendeleo.