Msemaji wa serikali Isaac Mwaura, amesema serikali itakata rufaa dhidi ya uamuzi wa hivi majuzi wa mahakama, uliopiga marufuku baraza la taifa la usalama kuwapeleka maafisa wa polisi nchini Haiti.
Mwaura alisema polisi wana uwezo unaohitajika wa kurejesha utulivu katika shemu yoyote ile ya dunia.
Akiwahutubia wanahabari siku ya Alhamisi, Mwaura alisisitiza kuwa Kenya ina rekodi nzuri ya historia ya kudumisha amani katika sehemu mbali-mbali duniani kote.
Mwaura alisema kuwapeleka maafisa wa polisi nchini Haiti, ni ishara kwamba Kenya inawaunga mkono wananchi wa Haiti wanaohangaika kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii kufuatia mzozo wa kisiasa nchini.
Rais William Ruto siku ya Jumanne alisema mpango wa kuwapeleka polisi 1,000 nchini Haiti, utaendelea licha ya uamuzi wa mahakama.
Kwenye mahojiano katika kongamano la Italia na Afrika, Rais alisema anaheshimu maombi ya Umoja wa Mataifa ya kuwapeleka polisi nchini Haiti kwa vyovyote vile.
Kwenye uamuzi uliotolewa Ijumaa wiki iliyopita, Jaji wa mahakama kuu, Chacha Mwita alisema hatua iliyopendekezwa ya kuwapeleka maafisa wa polisi ni kinyume cha sheria.
Aidha, alisema baraza hilo la kitaifa la usalama, halina mamlaka ya kuwapeleka maafisa wa polisi nchini Haiti, kuambatana na sheria, akisema, linaweza kuwapeleka wanajeshi pekee.