Home Habari Kuu Serikali kujenga kiwanda cha maziwa kaunti ya Narok

Serikali kujenga kiwanda cha maziwa kaunti ya Narok

Waziri alisema awamu ya pili ya mradi huo itahusisha ujenzi wa viwanda vya maziwa huko Mogotio na Kabianga.

0

Serikali kupitia kwa kampuni ya new KCC, itajenga kiwanda cha maziwa kwa gharama ya shillingi million 750 katika kaunti ya Narok, ili kuimarisha utoaji wa maziwa na mapato kwa wafugaji wa ngombe wa maziwa.

Akiongea wakati wa mkutano wa wakulima mjini Narok, waziri wa vyama vya ushirika na biashara ndogo ndogo na za kadri Simon Chelugui, alisema serikali inanuia kuangamiza wafanyabiashara walaghai wanaowanyanyasa wakulima kwa kununua maziwa kwa bei ya chini na kuyauza kwa bei ya juu.

Waziri pia alimuagiza mwenyekiti wa kampuni ya new KCC,David Maina,na afisa mkuu mtendaji, Nixon Sigey, kulainisha uuzaji wa maziwa katika kaunti hiyo ili wakulima wasipunjwe.

“Kwa kujenga viwanda hivi, tutasitisha uchuuzi wa maziwa, ambapo wakulima huuza maziwa kwa bei ya chini sana ya hadi shilingi 30 kwa lita moja. Bei ya ununuzi haitakuwa chini ya shilingi 50,” alisema Waziri huyo.

Alisema kaunti ya Narok ina uwezo wa kutoa zaidi ya lita elfu mia moja za maziwa kwa siku kwasababu ya hali nzuri ya hewa na ardhi kubwa ya malisho kwa mifugo.

Waziri alisema awamu ya pili ya mradi huo itahusisha ujenzi wa viwanda vya maziwa huko Mogotio na Kabianga.

‚ÄúTunalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji maziwa kutoka lita milioni 1.5 hadi lita milioni 4.5 kila siku kupitia kuwahamasisha wakulima,” alidokeza Waziri Chelugui.

Chelugui alisema hatua inatokana na agizo la Rais William Ruto kwa wizara yake, ijenge kiwanda cha maziwa, akiongeza kuwa Rais atazindua kiwanda hicho hivi karibuni.