Home Kaunti Serikali kujenga jumba la shilingi milioni 100 katika chuo cha KMTC

Serikali kujenga jumba la shilingi milioni 100 katika chuo cha KMTC

0

Serikali ya kitaifa kupitia kwa Wizara ya Afya na chuo cha matibabu nchini cha KMTC Nairobi, itajenga jumba la ghorofa nne litakalogharimu shilingi milioni 100 .

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika chuo cha matibabu eneo la Kocholia, mbunge wa Teso Kaskazini Oku Kaunya, alisema kuwa shilingi milioni 35 zitatumiwa kujenga ofisi za walimu, maabara mbili na ukumbi wa hadhara.

Awamu ya kwanza itakuwa kukamilisha ghorofa ya kwanza, huku mradi huo ukitarajwia kujengwa kwa awamu tatu.

“Hii ni sehemu ya mipango ya upanuzi wa chuo inayolenga kuunda nafasi zaidi ya kuchukua wanafunzi zaidi wanaojishughulisha na udaktari, uuguzi na kozi nyingine,” mbunge huyo alisema.

Mbunge huyo aliongeza kuwa mradi huo utaimarisha hali ya maisha ya jamii karibu na chuo hicho.

“Hii pia itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha jamii ya wakazi wanaoishi karibu na taasisi hiyo kupitia ujenzi wa bweni, wafanyabiashara wadogo na wachuuzi.”

Kaunya aliitaka Kampuni ya Ideal Construction yenye makao yake makuu Nairobi, iliyoshinda zabuni ya kufanya ujenzi huo kufanya kazi nzuri kwa muda uliotengwa.

Mbunge huyo pia aliwasilisha hundi ya shilingi milioni 5.3 msimamizi mkuu wa chuo, Daniel Kurui na naibu wake Cyrus Shivira,ikiwa hiyo ni sehemu ya shilingi milioni 10, ambao ni ufadhili kutoka hazina ya ustawishaji maeneo bunge (NG-CDF) kwa wanafunzi 120 wanaosomea kozi mbalimbali chuoni humo.

Alphas Lagat
+ posts