Serikali imebuni mikakati ya kuimarisha uzalishaji wa nyama ya ng’ombe, ili kukidhi soko la bidhaa hiyo.
Waziri wa kilimo Mithika Linturi, alidokeza kuwa Kenya bado haijatosheleza soko la nyama hapa nchini na hata kimataifa, na ipo haja ya kuwekwa juhudi za pamoja uzalishaji kabambe wa nyama ya ng’ombe.
Waziri huyo alielezea kujitolea kwa serikali kuongeza ufugaji wa ng’ombe nchini, kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa nyama na ngozi.
Aliyasema hayo alipozuru shamba la Mutara Ol-Pejeta katika kaunti ya Laikipia, akiwa ameandamana na katibu katika wizara hiyo Jonathan Mueke na Gavana wa Laikipia Governor Joshua, miongoni mwa viongozi wengine.
Linturi alisema wizara yake imechukua hatua za kuongeza mbegu za ng’ombe wa nyama, chanjo ya mifugo, kuwanonesha ng’ombe na lishe ya mifugo, ili kufufua sekta ya mifugo nchini kwa ushirikiano na serikali za kaunti na wafugaji wengine wa kibinafsi.
Kwa upande wake Gavana wa Laikipia Joshua Irungu,alipongeza juhudi za serikali za kukabiliana na magonjwa ya mifugo hasaa miongoni mwa jamii za kuhamahama.
Katibu katika wizara ya mifugo, Jonathan Mueke alidokeza kuwa punde tu sekta ya mifugo itakapoimarishwa, taifa hili halitaagiza bidhaa za ngozi kutoka nchi za kigeni.