Serikali inanuia kufufua mradi wa unyunyiziaji maji mashamba wa Halmashauri ya Maendeleo ya Mto Tana Athi, TARDA ambao ni mmoja wa miradi mikuu ya serikali ya Kenya Kwanza inayolenga kuongeza usalama wa chakula nchini.
Ekari elfu 50 zitatumiwa kwenye mradi huo kwa uzalishaji wa mchele na nyasi kavu.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, akizungumza wakati wa ziara ya kujionea mradi huo, alisema tayari umepokea shilingi laki nne za kukarabati mifereji na kwamba shilingi zingine milioni 300 zitatolewa ili kuongeza uzalishaji.
Alikuwa ameandamana na mwenyekiti wa TARDA Patrick Gichohi anayesema azima yao ni kuona mradi huo ukifufuliwa na kuongeza uzalishaji.
Serikali inapanga kuanzisha mpango wa uwekezaji kati ya sekta ya umma na kibinafsi ili kuongeza uzalishaji baada ya kuweka miundombinu ambayo itaziruhusu sekta za kibinafsi kushiriki mradi huo.
Koskei anasema Rais William Ruto ana malengo mwafaka ya kuhakikisha nchi hii ina chakula cha kutosha.
TARDA imekabidhiwa jukumu la kufanya kilimo cha uzalishaji mchele katika eneo la Delta ambacho tayari kimeanza katika ekari za kwanza 100.
Mchele tayari umevunwa katika eneo hilo ikiwa ni ishara bayana kuwa mradi huo utakuwa muhimu katika kuihakikishia nchi hii usalama wa chakula.
Ushirikiano wa sekta ya umma na kibinafsi utakuwa muhimu katika utekelezaji wa mradi huo ambapo wawekezaji wa kibinafsi wataruhusiwa kufanya uzalishaji na tayari mmoja ameruhusiwa kufanya kilimo hicho kwenye ekari 25,000.
Wakazi wana imani kuwa mradi huo utaleta mabadiliko katika eneo hilo ambalo linategemea mno kilimo cha unyunyiziaji maji mashamba.
Gorisso Golo ni mkazi wa eneo hilo anayetokea kijiji cha Banti. Anasema jamii zote katika eneo la Delta zinaunga mkono kufufuliwa kwa mradi huo na zitaunga mkono hatua yoyote inayolenga kuhakikisha wanapata ajira na chakula kwa ajili ya familia zao.