Home Kimataifa Serikali kufadhili shirika la JOYWO

Serikali kufadhili shirika la JOYWO

0
kra

Rais William Ruto amesema kwamba serikali inabadilisha muundo wa makundi ya uwekezaji na mikopo almaarufu “Table Banking” ili kuwezesha ukuaji wa biashara ndogo na za kadiri kupitia hazina ya Hustler.

Alisema kupitia hilo, serikali itaweza kusaidia ujumuishaji wa wote kifedha hasa makundi yaliyotengwa na ya watu walio katika mazingira magumu kama vile vijana na wanawake ambao wako chini kabisa katika mfumo wa kiuchumi.

kra

Rais Ruto aliahidi kwamba serikali itafadhili makundi ya wanawake chini ya shirika lao la Joyful Women Organisation – JOYWO.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 14 tangu kuasisiwa kwa shirika hilo, Rais Ruto alisema kwamba kila kundi chini ya shirika la JOYWO litaongezewa asilimia 100 ya pesa ambazo wamechanga.

“Pesa za Hustler Fund na pesa za women enterprise fund, katika kile kikundi chenu sasa, hazitakuwa ni zile pesa zenu peke yake mmewekeza, kama mmechanga shilingi elfu 100 tutawaongezea elfu 100,” alisema Rais.

Kuhusu mifumo dijitali, Rais alisema makundi yote ya shirika la JOYWO yatawezeshwa kuwa katika majukwaa ya kidijitali ambapo wanaweza kuendeleza biashara zao.

Shirika la JoYWO lilibuniwa na mkewe Rais Racheal Ruto miaka 14 iliyopita.

Sherehe za leo zilihudhuriwa na mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi, wake za Marais wa bara Afrika kama Monica Geingos wa Namibia, Rebecca Akufo-Addo wa Ghana, Angeline Ndayishimiye wa Burundi na Janet Museveni wa Uganda.

Viongozi wakuu serikalini pia walihudhuria hafla ya leo akiwemo Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi, Mawaziri Aisha Jumwa, Aden Duale, Susan Nakhumicha na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kati ya wengine.

Website | + posts