Home Biashara Serikali kubuni jopo kushughulikia changamoto katika sekta ya maparachichi

Serikali kubuni jopo kushughulikia changamoto katika sekta ya maparachichi

Naibu Rais Rigathi Gachagua amewaahidi wakulima wa maparachichi kwamba malalamishi yao yatashughulikiwa ili kuhakikisha wanapata faida ifaayo kutokana na kilimo hicho.

Aidha Naibu Rais alisema jopokazi litabuniwa la kuangazia kwa undani changamoto zinazowakumba wakulima wa maparachichi ili kuifanya sekta hiyo kuwa ya manufaa kwa wakulima.

Akizungumza jana alipokutana na wadau katika sekta ya kilimo cha maparachichi nyumbani kwake mtaani Karen, Gachagua alisema serikali imechukua hatua zifaazo kulinda sekta hiyo ya mamilioni ya pesa kufuatia lalama za wakulima kuhusu ushuru mpya unaotozwa zao hilo.

Ameongeza kuwa mazungumzo yanaendelea kuangazia upya kanuni za kisheria kwenye sheria ya fedha ya mwaka 2023 iliyoanzisha ushuru wa zao la maparachichi na kilimo cha mboga na matumda.

Naibu Rais alisema jopokazi hilo linatarajiwa kuratibu suluhu kwa matatizo yanayokumba sekta ya kilimo cha maparachichi.

Wanachama wa jopokazi hilo watakuwa wakulima, wauzaji zao hilo katika mataifa ya kigeni, wawakilishi wa kampuni za meli na maafisa wa serikali kutoka wizara husika.