Serikali inalenga kupunguza gharama ya kutuma fedha kutoka nchi za kigeni hadi humu nchini, ili kufanikisha mpango huo.
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, amesema kumekuwa na mazungumzo kwa mapana na marefu kuhusu haja ya kupunguza gharma hiyo kutoka kwa raia wanaoishi ughaibuni hadi katika mataifa wanakotoka.
Kulingana na Mudavadi aliyepia waziri wa mambo ya nje, serikali inashinikiza kuwezesha gharama za fedha zinazotumwa kutoka ng’ambo ziwe chini ya asilimia 3 ya thamani ya uhamisho wa fedha, kuambatana na malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG), sehemu ya 10 (c).
“Mazungumzo hayo yanajumuisha sera zitakazohakikisha kampuni zinazotoa huduma hizo zinatekeleza kikamlifu kiwango hicho ili kuwafaidi wanaolengwa na fedha hizo,” alisema Mudavadi.
Mudavadi aliyasema hayo katika taasisi ya mafunzo ya serikali, alipozindua mpango wa mkakati wa idara ya ughaibuni ambayo iko chini ya wizara yake.
Alisema pato kutoka kwa wakenya wanaoishi ng’ambo liliongezeka na kufikia dola bilioni 2.8 kati ya Januari na Julai mwaka 2024, ikilinganishwa na pato la dola bilioni 2.4 la kipindi sawia mwaka uliopita.