Home Habari Kuu Serikali kuanzisha vituo vya Huduma Centre katika maeneo bunge 290

Serikali kuanzisha vituo vya Huduma Centre katika maeneo bunge 290

0
Waziri wa Utumishi wa Umma Aisha Jumwa
Waziri wa Utumishi wa Umma Aisha Jumwa

Serikali inapanga kuanzisha vituo vya Huduma Centre 290 katika maeneo bunge yote katika juhudi za kupeleka huduma karibu na wananchi.

Waziri wa Utumishi wa Umma Aisha Jumwa amesema Huduma Kenya katika mpango wake wa kutoa huduma kwa njia ya kidijitali imepanga kuanzisha vituo 290 vya Huduma Centre katika maeneo bunge 290 kufuatia maombi kutoka kwa raia na viongozi.

Jumwa alisema vituo hivyo vitasaidia kuokoa mamilioni ya pesa zinazotumiwa na raia kutafuta huduma katika vituo vya Huduma Centre kwani vingi vya vituo hivyo vinapatikana katika makao makuu ya kaunti isipokuwa katika kaunti za Nairobi na Kajiado ambazo zina vituo 5 na 2 mtawalia.

“Mwaka huu, tutajenga vituo kadhaa vya Huduma Centre na tutafuta fedha zaidi za kujenga vituo hivyo katika kaunti ndogo ili kupeleka huduma karibu na raia,” alisema Jumwa.

Waziri aliyasema hayo leo Ijumaa jijini Mombasa alikofunga mkutano wa kwanza wa kila mwaka wa mameneja wa vituo vya Huduma Centre. Mameneja hao walishauriwa kubadilika na kukumbatia enzi ya dijitali.

Wizara ya Utumishi wa Umma inatafuta uwezekano wa kushirikiana na Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneo Bunge (NG-CDF) ili kufadhili uanzishwaji wa baadhi ya vituo vya Huduma Centre katika kaunti ndogo.

“Huduma Kenya inajulikana kama kiungo kinachoaminika kati ya raia na huduma za serikali na hiyo ndio sababu Huduma itadumu milele. Huduma Kenya ni sharti ipate mahali pake stahiki ili kupeleka huduma za kidijitali kwa watu,” alisema Jumwa.

Kuhusiana na utoaji huduma kwa njia ya dijitali, alipongeza uongozi wa Huduma kwa kuwa na ubunifu na kukumbatia enzi ya dijitali inayoendana na nguzo ya dijitali ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu (BETA).