Home Kimataifa Serikali kuanza ukarabati wa maghala ya NCPB kote nchini

Serikali kuanza ukarabati wa maghala ya NCPB kote nchini

0

Serikali hivi karibuni itaanza ukarabati wa maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao, NCPB kote nchini. Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei anasenma hatua hiyo inalenga kujiandaa kwa mavuno mengi ya mahindi. 

Koskei amesema serikali itakarabati vikausha mahindi sogevu 36 na kununua vingine 70 kama sehemu ya jitihada za serikali kuelekea usimamizi wa kipindi cha baada ya mavuno wa mazao ya wakulima.

“Katika kipindi cha miezi miwili ijayo, uhaba wa chakula utasahaulika,” alisema Koskei katika kanisa la AIC katika eneo la Kerotet, kaunti ya Uasin Gishu.

Aliongeza kuwa serikali ya kitaifa na zile za kaunti zitaboresha barabara katika eneo la  North Rift ili wakulima waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi hadi kwenye maghala ya NCPB.

“Serikali itawasaidia wakulima kutoka kiwango cha uzalishaji hadi usimamizi wa kipindi cha baada ya mavuno,” alisema Koskei.

Alitoa wito kwa wakulima kutotumiwa vibaya na mawakala na kuwashauri kuhifadhi mazao yao kwenye maghala ya NCPB wapendavyo wakisubiri bei za bidhaa hiyo kuimarika.

Kadhalika aliwataka kukumbatia mbinu za kisasa za kilimo ili kupata mafao bora kwa uwekezaji wao.

Kulingana na Koskei, serikali hivi karibunu itaanzisha awamu ya pili ya usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kote nchini.

Gavana wa kaunti ya Uasin Gishu Jonathan Bii na Seneta Jackson Mandago ni miongoni mwa waliokuwapo wakati wa hafla hiyo.

Website | + posts